TANGA YAWAKUMBUKA MASHUJAA
Na: Mussa Labani
Kitengo cha Mawasiliano serikalini Jiji la Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mhe. Hashim Mgandilwa leo Jumatatu Julai 25, 2022, amewaongoza wakazi wa Wilaya ya Tanga katika maadhimisho ya siku ya mashujaa iliyofanyika katika bustani ya uhuru (Uhuru Park) katikati ya Jiji la Tanga.
Maadhimisho hayo ambayo yamehudhuriwa na askari wastaafu walioshiriki vita mbalimbali za ukombozi na utunzaji wa amani, ikiwemo vita ya kumaliza uchokozi wa Idd Amin wa Uganda na Tanzania, utunzaji wa amani huko Darfur, na maeneo mengine, yalianza kwa sala na dua kutoka kwa viongozi wa dini.
Katika dua na sala zao, viongozi hao wa kidini, Sheikh wa Mkoa wa Tanga Ally Juma Luwuchu wa Baraza la Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), MT 30580 SGT Mstaafu Joseph Mhilu wa Kanisa la Anglikana, na Fr. Joseph A. Mbena wa Kanisa Katoliki Tanga, wamewaombea dua na kusihi watanzania kudumisha amani.
Akitoa hutuba fupi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Mgandilwa amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa na wazee waliojitoa kuipigania nchi na kujenga amani ambayo tunapaswa kuilinda na kuienzi.
Mgandilwa amesema tunapaswa kuwa na moyo kama wa wazee wetu, amesema wazee wetu wamefanya wajibu wao kuhakikisha Tanzania inakuwa salama.
"Tunatakiwa tudumishe amani tuliyo nayo kama njia ya kuwaenzi hawa wenzetu. Vinginevyo tutakuwa hatuwatendei haki wenzetu waliotangulia mbele za haki. Nchi yetu ipo salama, ni njema tukabainisha ile mianya yote inayoweza kupelekea uvunjifu wa amani. Tuibaini na tuizuie." Ameasa Mheshimiwa Mgandilwa.
Awali, mwakilishi wa mashujaa Mzee Stephen Ignatius Mponji ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka na kuendelea kuuenzi mchango wao katika ujenzi wa taifa, huku akiwaasa askari walio makambini kuzingatia mazoezi, ukakamavu na nidhamu.
"Sisi tulijitoa mhanga, tuliisaidia nchi yetu kile kipande cha ardhi kilichotekwa pale Kyaka. Niwasisitize wapiganaji mlio kambini, mzingatie mafunzo na nidhamu, nasisitiza ni muhimu sana" amesisitiza Mzee Mponji.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe Abdulrahman Shiloow, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Ndg. Sipora Liana, Katibu Tawala Wilaya ya Tanga, Ndg. Dalmia Mikaya, Viongozi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Watumishi wa Jiji la Tanga pamoja na wananchi kwa ujumla.
Baada ya maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya aliwaongoza viongozi kwenda hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo, kumjulia hali Mzee Mbega Salum mkazi wa Magomeni aliyeshiriki vita ya pili ya dunia aliyelazwa katika hospital hiyo, akikadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 95 na 102, huku Mkurugenzi wa Jiji akiwashika mkono askari mashujaa waliohudhuria shughuli hiyo.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.