Katika kutekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Walemavu mkuu wa mkoa wa Tanga Mhe.Martine Shigela amekabidhi pikipiki 70 kwa vijana wanaounda kikundi cha Tanga One Youth Group (TOYG).
Akikabidhi pikipiki hizo zenye thamani ya shilingi Mil.182, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martine Shigela amesema amefurahishwa kuona Tanga jiji inaendelea kuwa kinara kwa utoaji mikopo kwa kata zote 11 alizotembelea kwa vijana ,wanawake na walemavu ambao wamepewa mikopo .
“Ninafuraha kuona Tanga Jiji imeendelea kuwa kinara kwa utoaji wa mikopo kwa kata za Halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga na leo tumeshuhudia vijana hawa wamekabidhiwa pikipiki hizi na kwa kila kata mmetoa kwa wanawake ,vijana na walemavu”.Amesema Mhe Martine Shigela Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Ameongeza kuwa mikopo hiyo haina riba hivyo watarudisha pesa zilezile walizokopa na amewataka waliochukua mikopo kuitumia vizuri ili waweze kuirejesha na wengine kukopa.
Pia amesema amefarijika kuona Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani ametoa mafunzo kwa vijana hao kabla hawajakabidhiwa pikipiki hizo hivyo hategemei tena kusikia kesi zozote kama kipindi cha nyuma .
Akisoma taarifa Afisa Maendeleo wa Jiji Bi .Dorah Ntumbo amesema kikundi hicho kimesajiliwa Aprili 30 na kupewa namba za usajili Tcc/Kkd/2019/067, kikundi hiki kinajishugulisha na uendeshaji wa pikipiki za usafirishaji wa abiria.
“Mhe Mkuu wa Mkoa ili kufanikisha malengo ya kikundi hiki Halmashauri ya Jiji la Tanga imetoa mkopo wa jumla ya Tshs Mil. 182 kwaajili ya ununuzi wa pikipiki 70 kwa ajili ya vijana na kwa kushirikiana na kamanda wa usalama barabarani vijana hawa wamepewa mafunzo ya usalama barabarani Ujasiriamali pamoja na Ofisi ili waweze kufanya kazi”.Alisoma Afisa Maendeleo ya Jiji Bi Dorah Ntumbo
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga Ndg Solomoni Mwangamilo amesema wameamua kuwapa mafunzo hayo ili waweze kuwa watiifu katika sheria na wafuate taratibu na kanuni za usalama barabarani.
“Kuendesha pikipiki imekuwa sehemu kubwa sana ya kuvunja sheria kwa sababu waharifu wengi wanatumia pikipiki, hivyo tumewapa mafunzo hayo ili waweze kuwabaini waharifu na kuwajengea uwezo wa wao kutoa taarifa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake”.Amesema Mkuu wa Usalama barabarani Solomoni Mwangamilo
Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga jumla ya Tshs 800,449,700/=kwa ajili ya mikopo kwa wanawake,walemavu,na Vijana ,ambapo vijana wametengewa jumla ya 355,094,000 /= na hadi kufikia juni 2019 jumla ya Tshs 353,000,000/= zimetolewa kwa vikundi 20 vya vijana wa Jiji la Tanga .
Baadhi ya Vijana wakiwa kwenye Pikipiki walizokabidhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martine Shigela akiwa amekaa kwenye Pikipiki.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Ndugu Daudi Mayeji akiongea katika makabidhiano ya Pikipiki hizo.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.