Na. Mussa Labani. Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba amesema yupo tayari kuanza kazi baada ya kuhitimisha ziara ya kujitambulisha kwa Wilaya na Halmashauri za mkoa wa Tanga.
Mgumba ameyasema hayo alhamisi Septemba 8, 2022 wakati akihutubia Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Jiji la Tanga uliokuwa na lengo la kujitambulisha kwa Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Jiji, ikiwa ni kituo cha mwisho cha ziara yake.
Akihutubia mkutano huo, Mgumba amelipongeza Jiji la Tanga kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuongoza majiji mengine hapa nchini katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa kukusanya mapato kwa asilimia 113 ya lengo la mwaka.
Mgumba amesema dhana ya ugatuaji madaraka inataka Halmashauri kujikusanyia mapato na kutoka kwenye utegemezi wa kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu.
Amesema Halmashauri zinapaswa kuondoka kwenye mazoea ya ujenzi wa madarasa, vyoo na vituo vya afya pekee, na kuanza kufikiri kuwa na miradi ya kiuchumi itakayo kuwa chanzo cha mapato badala ya kusubiri kukusanya ushuru pekee kwa wananchi.
"Mapato ni kipaumbele cha pili baada ya usalama. Na mapato haya yaende kutatua shida za wananchi. Mtu asijaribu kucheza na fedha hizi, Mheshimiwa Rais amekwisha sema, ukitaka kujua rangi yake, basi chezea fedha hizi." Amesema Mgumba.
Mheshimiwa Mgumba ambaye aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliwataka Madiwani kuhakikisha kunakuwa na msawazo/mtawanyo wa fedha za utekelezaji wa miradi ili kila kata ipate mradi kwa maendeleo ya wananchi, badala ya miradi mingi na mikubwa kuwekwa katika kata moja, huku akishauri utengaji wa fedha uwe wa kutosha kukamilisha mradi ili kuwezesha huduma kutolewa kwa wananchi.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Jiji la Tanga kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Jiji Ndg. Sipora Liana amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 unaoishia mwezi Juni 2022, Halmashauri imefanikiwa kupeleka katika miradi mbalimbali ya maendeleo zaidi ya shillingi billion 6.6 ikiwa ni katika utekelezaji wa utoaji wa asilimia 60 ya mapato ya ndani.
"Kati ya fedha hizi, shillingi 1.1 billion zimeelekezwa katika sekta ya afya, shillingi 2.7 billion sekta ya elimu, shillingi 167 million zimepelekwa eneo la utawala katika ujenzi wa ofisi za kata, na utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu ni 1.1 billion, sekta ya biashara ikitengewa million 100 kwa ajili ya ujenzi wa soko, shillingi 410 million zikitumika katika shughuli za anwani za majazi, na miradi mingine ya uwekezaji na ufuatiliaji ikigharimu shillingi 995 million". Amefafanua Liana.
Mkutano huo maalum wa Baraza la Madiwani uliongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloow, ulihudhuriwa na viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.