Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Hashim Mgandilwa ameagiza kukamilika kwa miradi yote ya ujenzi inayotekelezwa ndani ya jiji la Tanga hadi kufikia julai 30, mwaka huu.
Ameyatoa maagizo hayo Jumanne Julai 12, 2022, katika siku ya pili ya ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tanga ya kukagua utekelezaji wa miradi na kujua changamoto zinazochelewesha ukamilishaji wa miradi, ambapo ameonyesha kutokuridhishwa na utendaji wa baadhi ya mafundi (local fundi) wanaofanya kazi kwa utaratibu wa "force account".
Mheshimiwa Mgandilwa ameagiza kupunguzwa kwa idadi ya miradi kwa fundi wenye miradi zaidi ya mitatu katika maeneo tofauti, na kupewa fundi wengine, ili kuwezesha miradi hiyo kwenda haraka badala ya kujaza kazi kwa fundi mmoja, ambapo imeonyesha kutoleta tija kwa miradi.
"Kwanza naipongeza Halmashauri, Madiwani, Mbunge na Mkurugenzi kwa upelekaji mzuri wa fedha nyingi sana katika miradi. Sasa fedha zipo, na tuna miradi mingi. Natamani kuona miradi inakamilika, tufanye miradi mingine" amesema Mheshimiwa Mgandilwa.
Katika ziara hiyo ya siku tatu, Kamati ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya inatembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambapo katika siku yake ya pili ilianzia shule ya Msingi Kombezi iliyopo kata ya Makorola, na kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya darasa na ofisi vinavyojengwa kwa fedha za mradi wa GPE - LANES kiasi cha shillingi million 40.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Paulina Nyagawa amesema shule hiyo ina wanafunzi 794 na kila darasa lina mkondo mmoja - mmoja hivyo upatikanaji wa vyumba hivyo vya madarasa vitawezesha wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kugawanywa katika mikondo ya miwili.
"Ndugu Mgeni Rasmi, mpaka sasa tumeshatumia shilling million 32,922,775 na tumebakiwa na shillingi 7,077,225 kwenye akaunti ikiwemo hela ya fundi shillingi 2,986,475 kumkamilishia gharama zake za ufundi, na tutabaki na shillingi 4,090,750 ambayo tunaomba kununua madawati 16 na viti 10 meza za walimu 15 na kabati dogo" ameongeza Mwalimu Nyagawa.
Ziara hiyo iliyowahusisha baadhi ya wakuu wa idara za Halmashauri, ilipita katika miradi tisa ambapo kati yake, miradi minne ikiwa ni ya elimu, afya ni miradi mitatu na miradi miwili ni ujenzi wa nyumba za watumishi.
Ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama inatarajiwa kuhitimishwa siku ya jumatano, na siku ya alhamisi kamati hiyo inategemewa kuungana na wakazi wa mtaa wa Geza, kata ya Marungu katika zoezi la uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa Zahanati.
Labani.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.