Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Mhe. Al-Hajj Abdulrahman Shiloow ameitaka Halmashauri hiyo kuanza utaratibu wa kutenga fedha katika bajeti yake ya mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki za Watendaji wa Kata kwa kuanzia na Kata zilizo pembezoni na zenye mazingira magumu ya usafiri.
Al-Hajj Shiloow ameyasema hayo leo, Jumanne, Februari 21, 2023 wakati akikabidhi pikipiki kwa Mtendaji wa Kata ya Pongwe Jijini Tanga Bi. Erica Njama ikiwa ni moja ya pikipiki 916 zilizotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa lengo la kusaidia usafiri kwa Watendaji wa Kata nchini, na kukabidhiwa kitaifa hivi karibuni na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Isdor Philip Mpango, ambapo Halmashauri ya Jiji la Tanga imepata pikipiki moja.
Shiloow amesema zipo Kata kubwa na zilizo mbali, ambazo nazo zinahitajika kupata pikipiki akitolea mfano wa kata ya Maweni, Mabokweni na Chongoleani, huku kata za Kirare na sasa Pongwe tayari zikiwa zimepata usafiri huo.
"Jiji ni kama tumekumbushwa (kwa Serikali kutoa pikipiki kwa Watendaji wa Kata), uwezo tunao lakini hatuweki kipaumbele cha kununua pikipiki. Uwezo wa kununua pikipiki 2 au 3 kila mwaka tunao. Tuliangalie hili kwa kuweka kwenye bajeti zinazokuja ili kila mwaka tupunguze idadi ya Watendaji wanaohitaji pikipiki" amesisitiza Shiloow.
Kwa upande wake Bi. Erica Njama, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia usafiri Watendaji wa Kata utakao wasaidia katika kutekeleza shughuli za kila siku za kuihudumia jamii.
"Nimekuwa nikipata changamoto za kiutendaji kwa sababu kata ya Pongwe ni kubwa na kuna maeneo kuyafikia ni umbali wa kilomita 25 hadi 30. Wakati mwingine unapigiwa simu kuwa kuna tatizo sehemu, lakini huwezi kufika kwa wakati kwa kukosa usafiri.
Ila kupitia chombo hiki ambacho Mheshimiwa Mama yetu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia, basi, mimi kama mtumishi wake, nitakwenda kuitumia pikipiki hii kuhakikisha nawafikia na kuwatumikia wakazi wa Pongwe" amesema Njama.
Katika makabidhiano hayo, Mstahiki Shiloow amemkabidhi Bi. Njama pikipiki aina ya Boxer, pamoja na kofia ngumu (Helmet) huku akimtaka kukitunza kifaa hicho na kutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Tukio hilo lililofanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Tanga lilihudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji Bi. Hawa Msuya, Afisa Utumishi Mkuu wa Jiji Bi. Mwanaidi Nondo, na viongozi wengine. Ambapo pikipiki hizo zinakusudiwa kuwawezesha Maafisa hao kuwafikia wananchi kwa urahisi kwa lengo la kuwahudumia na ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika kata zao.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.