Viongozi, Wafanyakazi na wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Tanga, leo wamejumuika kwenye uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga kusherehekea sikukuu ya wafanyakazi duniani, Mei Mosi.
Kama ilivyo kawaida wa sherehe hizo, huwa na michezo mbalimbali ambapo washindi wa michezo hiyo pamoja na wafanyakazi hodaria kutoka kwenye taasisi mbalimbali walipewa zawadi na mgeni rasmi, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga (DC TANGA) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Kabla ya kutoa zawadi hizo kwa washindi, ilisomwa risala ya shirikisho la wafanyakazi Tanzania, (TUCTA ) kwa mgeni rasmi ambayo ndani yake kulikuwa na hoja zilizohusu masuala ya mahitaji na maboresho ya maslai ya wafanyakazi.
Akitolea maelezo baadhi ya hoja zilizowasilishwa kwenye risala hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Thobias Mwilapya, alianza kwa kuwashukuru wafanyakazi kwa pongezi nyingi walizompa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufi. Mgeni rasmi huyo aliwaahakikishia wafanyakazi ya kwamba serikali inafahamu mahitaji ya wafanyakazi wake na imeanza kuyafanyia kazi.
“Nia ya serikali ya kupungiza makato ya mshahara wa mfanyakazi hadi kufikia single digit bado ipo, kwa sasa wafanyakazi wanaopata mshahara chini ya laki saba, wameanza kupata punguzo hilo, kwa maana wanakatwa 9% kama kodi." Alisema mkuu huyo akitolea maelezo hoja ya kodi kubwa wanaokatwa watumishi kwenye mishahara yao.
Akizungumzia suala la wafanyakazi kuanzisha matawi ya vyama vya wafanyakazi kwenye maeneo yao ya kazi, Mhe Mwilapya alisema kwamba hii ni haki ya wafanyakazi na ipo kisheria. "Ni marufuku muajiri kumzuia mfanyakazi kujiunga kwenye chama cha wafanyakazi ama kuanzishwa kwa tawi wa chama cha wafanyakazi maana wafanyakazi wana haki ya kufanya hivyo" alisema Mhe Mwilapya. Sambaba na hili, alisisitiza waajiri wote kuwasilisha michango yao kwenye mfuko wa fidia wa wafanyakazi kama inavyosemwa kwenye sheria.
Katika nasaha zake kwa wafanyakazi, Mhe Mwilapya aliwaasa wafanyakazi kuwa na maadili mema na hatarajii kuona wala kusikia mfanyakazi anajihusisha na matendo yasiyo kuwa ya maadili, kama kujihusisha na magendo, kufanya biashara haramu na ubadhulifu wowote.
Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi huwa zinasherehekea duniani kote siku ya tarehe moja ya mwezi wa tano kila mwaka. Kitaifa sherehe hizi zilifanyika Manispaa ya Iringa ambapo Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania alikuwa mgeni rasmi.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.