Mussa Labani, Tanga.
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wanaounda Kamati ya Mipangomiji na Mazingira, wameeleza kuridhishwa kwao na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga, pamoja na ile ya ufadhili wa Taasisi ya Botnar Fondation.
Akiongea wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofanywa na Kamati hiyo, jumatano, Januari 11, 2023, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Habib N. Mpa amesema wameridhishwa na kazi zinavyoendelea na kuwa kukamilika kwa miradi kutasaidia kutatua changamoto mbalimbali, akitolea mfano wa maboresho makubwa yanayofanywa katika bustani ya Jamhuri, maarufu kama Forodhan.
"Tunaitengeneza bustani yetu ya Jamhuri, iwe ya kisasa, na Mwenyezi Mungu akijalia, itabadilisha Jiji la Tanga. Wananchi watafurahi, sio ile bustani walioizoea ya miembe na vibanda viwili." Ameongezea Mhe. Mpa.
Na kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Anjelika Nyangasa ametoa wito kwa jamii kuhakikisha wanatunza mazingira na miradi katika maeneo yao ili itumike na kwa faida ya vizazi vijavyo.
Kamati ya Mipangomiji chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Mpa, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngamiani Kati, imetembelea mradi wa uuzaji wa viwanja Mkurumuzi, ambapo katika eneo hilo kulikuwa na maboresho ya viwanja 1757 na waliolipia maboresho wakiwa ni watu 612 na huku taratibu za kuwachukulia hatua za kisheria zikiandaliwa kwa ambao bado kulipa.
Kamati ilikagua matengenezo ya greda la Halmashauri, kutembelea eneo la fukwe ya kuogelea (Raskazone beach) inayomilikiwa na Jiji, pamoja na ujenzi wa bustani ya Jamhuri maarufu kama Forodhan.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.