KAMATI ZA MADIWANI JIJI TANGA ZAANZA UKAGUZI WA MIRADI.
Na: Mussa Labani
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Jiji la Tanga
Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, leo Jumatatu Julai 25, 2022 imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi iliyo chini ya Idara zinazosimamiwa na kamati hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya vikao vya kamati vya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Ziara ya Kamati hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Habib N. Mpa, ambaye ni Diwani wa Kata ya Ngamiani Kati, ambapo kamati ilitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Maweni, na kisha kamati ilikwenda mtaa wa Kwakaheza A na B kuona maendeleo ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha (KKK).
Katika eneo la Maweni lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, kamati iliweza kuona eneo la mita za mraba 5132, ambapo kulingana na sheria, ujenzi wa kituo cha afya unahitaji eneo la kuanzia mita za mraba 5000.
Ziara hiyo ambayo ilimjumuisha Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloow, pamoja na wajumbe wengine wa kamati, na baadhi ya wakuu wa idara za Halmashauri, ilipokea taarifa ya mradi wa KKK kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na wananchi kusimamia zoezi hilo, Mhe. Mzamil Shemdoe (Naibu Meya mstaafu na Diwani mstaafu wa kata ya Mabawa), ambaye alisema mtaa wao una jumla ya nyumba 648, ambapo nyumba kamili ni 600 na maboma 48.
Amesema kati ya nyumba 648, waliolipa ili kufanyiwa upimaji na urasimishaji ni 152 ambapo gharama kwa kila kiwanja ni shilingi 130,000.
"Tunajitahidi na kamati yangu kuhamasisha ili watu walipe. Kamati tunakutana kila wiki na tunagawana nyumba za kufuatilia. Hatutaki Mtaa wetu uwe sababu ya zoezi hili kukwama." Amesema Shemdoe.
Zoezi la KKK katika mtaa huo linafanywa na kampuni ya GeoPlan(EA) LTD na zoezi hili linafanyika katika mitaa kumi ndani ya jiji la Tanga, likitekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Serikali kuu kiasi cha shillingi million 400 ambapo fedha zinazolipwa na wananchi zinarejesha kiasi hicho cha mkopo.
Ziara ya kamati ya Mipango Miji na Mazingira imefungua ziara za kamati zingine za kudumu za Baraza la Madiwani ambapo siku ya Jumanne, Julai 26, 2022, Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu itafanya ziara na kufuatiwa na kamati ya Kudhibiti UKIMWI (CMAC) siku ya alhamisi Julai 28, na Kamati ya Fedha na Uongozi ikiwa ni Ijumaa, Julai 29, 2022.
Ziara hizi zinawapa nafasi Madiwani kuona kwa uhalisia hatua za utekelezaji wa miradi, ubora wa miradi na kujua changamoto za utekelezaji kabla ya kuingia kwenye vikao vya maamuzi katika kuleta ustawi wa jamii ya wakazi wa Jiji la Tanga.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.