Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), leo Jumatatu, Februari 27, 2023, imepokea wasilisho la rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa mwaka wa fedha 2023/2024, yenye makisio ya makusanyo na matumizi ya shillingi Billion 72,111,627,000.00 kwa lengo la kushauri maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wake.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hashim Mgandilwa amewataka wajumbe kufikiri na kutoa ushauri kwa Halmashauri namna ya kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa kuibua vyanzo vipya vya mapato, na kuwekeza katika miradi itakayozalisha mapato endelevu.
"Sisi kwa umoja wetu ndio wenye wajibu wa kutoa mipango, kwa kuangalia tunahitaji Tanga ya namna gani. Tupitie mapendekezo ya bajeti waliyotuletea na tuweze kupendekeza yale tunayofikiri yatakwenda kuijenga Tanga tunayoitaka." Amesisitiza Mgandilwa
Awali, akiwasilisha Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mkuu wa Sehemu ya Mipango na Ufuatiliaji Bw. Simeon Vedastus amesema kati ya shillingi Billion 72.1 zitakazo kusanywa, Billion 19.1 ni mapato ya ndani, ambapo asilimia 70 ya fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Sipora Liana amesema Jiji limetekeleza miradi mingi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 100 kwa shillingi Billion 2, huku akiwataka Watendaji wa Kata kuhamasisha wana vikundi vya kiuchumi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kujitokeza kuomba mkopo wa kuanzisha viwanda vidogo kwani fedha zipo kuwezesha makundi hayo.
Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe, Mstahiki Meya Al-Hajj Abdulrahman Shiloow amesema Halmashauri tayari inaendesha shule mbili za mchepuo wa kiingereza, na inakusudia kujenga shule zingine mbili, moja ikiwa Maweni njia ya Korogwe, na nyingine itajengwa njia ya Pangani.
Kikao hiki ni muendelezo wa vikao vya kupitia rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kabla ya kuwasilishwa katika Mkutano maalum wa Bajeti wa Baraza la Madiwani.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.