Mussa Labani, Tanga.
Wanafunzi wa Kidato cha kwanza waliojiunga na elimu ya Sekondari wiki hii katika Jiji la Tanga, wametakiwa kukataa vishawishi vyenye lengo la kuwaingiza katika mtego wa ngono, unaoweza kuwakatishia ndoto zao kwa kupata mimba katika umri mdogo na maambukizi ya UKIMWI.
Ushauri huo umetolewa na Kamati ya kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Tanga(CMAC), chini ya Mwenyekiti wake, Naibu Meya wa Jiji Mhe. Mwanaidi Kombo Chombo, leo jumanne Januari 10, 2023 wakati Kamati hiyo ilipotembelea shule ya Sekondari ya Horten iliyopo kata ya Duga kuzungumza na wanafunzi hao juu ya elimu ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi na vitendo vya kikatili kwa watoto.
Akizungumza na wanafunzi hao, Naibu Meya Mhe. Kombo amewataka wanafunzi hao, ambao bado ni watoto kutojiingiza katika kufanya ngono na iwapo mtu yoyote akimshawishi atoe taarifa mapema.
"Tusikubali kuharibu afya zetu. Mtapata ujauzito katika umri mdogo. Mtu yeyote akikushawishi, hata kama ni mjomba, bodaboda, dereva wa Hiace, yoyote, toa taarifa". Amesisitiza Mhe. Kombo.
Kamati imefanya ziara yake ya kawaida kutembelea shughuli na wadau, katika kudhibiti Ukimwi, ikiwa ni maandalizi ya kikao chake cha robo ya pili ya mwaka 2022/2023.
Kamati ilianza ziara kwa kutembelea Kamati ya kudhibiti UKIMWI kata ya Mabawa, baadae ikaelekea Shule ya Sekondari Horten, kituo cha Afya Duga na kumalizia kwa kutembelea Dawati la Polisi Chumbageni.
Shule ya Sekondari ya Horten ina wanafunzi 1775, na kwa mwaka huu wanafunzi wa kidato cha kwanza wanatarajiwa kuwa 550 na tayari wanafunzi 459 sawa na asilimia 83.4 wamekwisha ripoti kuanza masomo.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.