Halmashauri ya Jiji la Tanga imefanikiwa kuongeza kiwango cha utoaji wa fedha za mikopo kwa vikundi vya kiuchumi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kutoka katika asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shillingi Billion 2,088,530,000.00 zimetolewa kama mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo ili kuwawezesha kiuchumi, kulinganisha na Million 943 kwa mwaka 2020/2021.
Kiwango hicho cha fedha, kinajumuisha fedha zilizopangwa kutoka Bajeti ya mapato kwa mwaka huo, kiasi cha Billion 1,115,607,800.00 pamoja na fedha za marejesho ambazo nazo zimeingia katika mzunguuko wa ukopeshaji.
Akikabidhi mfano wa hundi zenye thamani ya shillingi million 377 kwa vikundi 43 (Wanawake vikundi 31 wakipokea jumla ya shillingi million 266, Vijana vikundi 6 Tsh. 83 M na wenye ulemavu vikundi 6 Tsh. 28 M), ambapo vinahitimisha awamu ya nne ya utoaji kwa mwaka 2021/2022, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloow amewataka wanavikundi hao kuzingatia mipango yao na kufanya biashara zenye tija ili warudishe mkopo na kupata faida ya kazi na kubadili hali zao za maisha.
Amesema fedha hizo sio za bure, ni mkopo, hivyo wanapaswa kufanya utafiti wa biashara sio kuiga kwa mwingine.
Mheshimiwa Shiloow ambaye alikabidhi hundi hizo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, aliwataka wakazi wa Jiji la Tanga kuwa na imani na Mbunge wao kwa jinsi anavyofanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo, na kwamba kila shughuli ya maendeleo, mkono wake upo, na kwamba alipenda awepo katika tukio hilo.
Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Sipora Liana alisema vikundi vinavyopata mkopo safari hii vimetumia njia ya mtandao katika kujaza taarifa zao na kwamba elimu na mafunzo yametolewa kwao na maafisa kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Tanga Bw. Simon Mdende amesema hali ya marejesho inakwenda vizuri na kwamba vipo vikundi vilivyomaliza mkopo na sasa wanapata kwa awamu ya pili.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.