BUSTANI YA JAMHURI KUJENGWA UPYA.
Mkataba wa kazi ya ujenzi wa bustani ya kupumzikia ya Jamhuri (Jamhuri Park) maarufu kama Forodhani iliyo kando ya bahari ya Hindi pembeni ya maktaba ya Mkoa wa Tanga, umewekwa saini na tayari mkandarasi amekabidhiwa eneo kwa kuanza kazi za ujenzi wa bustani hiyo.
Ujenzi wa bustani hiyo ni moja wa miradi mikubwa inayotekelezwa katika Jiji la Tanga kwa ufadhili wa Taasisi ya Botnar Fondation kupitia mradi wa Tanga Yetu, na unatarajiwa kugharimu kiasi cha karibu shillingi Billion mbili za Kitanzania.
Lengo la mradi huo ikiwa ni kuboresha sehemu za mapumziko kwa familia, na ambapo vijana wataweza kupata fursa ya kufanya biashara zitakazo waongezea kipato na hivyo kujikimu kimaisha.
Ujumbe wa wasimamizi wa mradi huo ESRF (Economic and Social Research Foundation), Ijumaa Julai 22, 2022 uliwaongoza wakandarasi wa mradi huo kampuni ya V. J. Mistry & Co. LTD ambao ndio walioshinda zabuni ya ujenzi, pamoja na Mhandisi Mshauri wa mradi kuwatambulisha kwa Mkurugenzi wa Jiji na Mstahiki Meya wa Jiji.
Akiongea na ugeni huo Ofisini kwake, Mkurugenzi wa Jiji Ndg Sipora Liana, amemtaka Mkandarasi V. J. Mistry kuhakikisha anaanza kazi mara moja na kukamilisha kazi kwa wakati.
"Hii kazi tumeisubiri kwa muda mrefu sana. Hivyo muanze kazi mara moja na mkamilishe kwa wakati. Tena ujenge hivi hivi kama inavyoonekana kwenye mchoro" alisisitiza Mkurugenzi Liana.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji, Mhe. Abdulrahman Shiloow amewataka wakandarasi kuwatumia vijana wa Tanga katika kazi ambazo hazihitaji utaalamu maalum.
"Katika zile nafasi za kazi ambazo sio "professional" hatutarajii kuona unaleta watu kutoka Dar es Salaam wakati hapa Tanga tuna vijana wengi tu. Kwa zile za kitaalamu, sawa. Lakini hizi zingine, vijana wa hapa Tanga wapate nafasi. Na pia nikukumbushe suala la kutoa CSR, unarudisha kwa jamii kile ulichopata, kwa kiwango kilicho ndani ya uwezo wako" amesisitiza Meya Shiloow.
Mradi wa ujenzi wa uboreshaji wa bustani ya Jamhuri(Forodhani) unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya kupatikana kwa mkandarasi, na shughuli za ujenzi zitakapoanza eneo litafungwa kulingana na mpango kazi wa mkandarasi.
Kukamilika kwa ujenzi wa bustani hiyo kutabadili kwa kiasi kikubwa muonekano wa eneo hilo la Jiji na kufanya mji kupendeza zaidi.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.