Na; Mussa Labani, Tanga.
Mtaa wa Jaje katika Kata ya Duga Jijini Tanga umeanza maandalizi ya ujenzi wa Shule mpya ya Msingi na madarasa ya awali itakayojengwa katika Mtaa huo, pembeni ya Shule ya Msingi Jaje kupitia fedha za mradi wa kuboresha upatikanaji wa fursa sawa katika ujifunzaji bora wa Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST), ambapo mtaa huo umepokea kiasi cha shillingi million 540,300,000.00 kwa ujenzi wa shule hiyo ya mikondo miwili yenye vyumba viwili vya madarasa ya elimu ya awali, pamoja na miundombinu yote ya shule ikiwemo vyoo.
Katika hatua za awali, Jumatatu, Mei 8, 2023, Kamati ya Utekelezaji Mradi wa Boost ya Jiji la Tanga, imeshiriki kikao cha kamati ya maendeleo ya Kata (WDC) na Mkutano wa Mtaa wa Jaje wenye lengo la kuutambulisha mradi, kuelimisha jamii na kuwataarifu kuhusu mapokezi ya fedha kwenye shule yao, shughuli iliyoenda sambamba na uchaguzi wa wajumbe wawakilishi wa jamii katika timu ya mradi ambao walipatikana kwa kuchaguliwa na mkutano huo.
Mkutano huo ulioendeshwa na mwenyekiti wa Mtaa huo, Ramadhan Omary, ulihudhuriwa pia na Diwani wa Kata ya Duga, Mhe. Jaffar Mohamed, ulihusisha wakazi wa mtaa huo, wadau wote wa eneo la mradi, wakiwemo viongozi wa dini, taasisi, makampuni, n.k., ambapo walipata wasaa wa kupata maelezo ya mradi, na fursa ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu.
Akitoa salamu za wakazi wa Kata, Mhe. Jaffar amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia kata hiyo shule mpya, ambapo amesema kwa sasa kata ina shule nne za Msingi lakini bado watoto ni wengi hivyo ujenzi wa shue mpya, itasaidia kupunguza tatizo la mrundikano wa watoto katika madarasa.
Aidha Jaffar amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Sipora Liana kwa jitihada zake za kuhakikisha eneo kwa ujenzi wa shule linapatikana na hivyo kuwezesha taratibu za ujenzi huo kuanza.
Ujenzi wa Shule hiyo unatekelezwa kwa mfumo wa Lipa kwa Matokeo (P for R) na unatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo tarehe 30 Juni, 2023.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.