Na; Mussa Labani, Tanga.
Halmashauri ya Jiji la Tanga imeendelea kutekeleza jukumu la udhibiti taka zinazozalishwa ili zisilete madhara kwa Jamii, kwa kuhakikisha magari ya uchukuzi taka yanaondoa taka na kuzipeleka dampo, na huku ikiendelea kusajiri vikundi vya taka ni mali vinavyojihusisha na urejerezaji (recycling) taka.
Hivi karibuni, wakati Mwenge wa Uhuru 2023 ulipopita katika Wilaya yetu, moja ya kazi zilizofanywa na Mwenge wa Uhuru, ilikuwa ni pamoja na uzinduzi wa gari jipya la kubeba taka la Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Gari hili (pichani) tayari lipo mtaani likiendelea na kazi hiyo, ikiwa ni moja ya mipango ya Halmashauri ya ununuzi wa magari ya kubebea taka ili kurahisisha kazi ya uondoaji wa taka katika mitaa.
Pamoja na ununuzi wa gari hilo, Halmashauri inafanya matengenezo ya vifaa na magari mengine ili kuongeza nguvu katika eneo hilo, huku ikijipanga kununua magari ya kisasa zaidi ya kubeba taka, na kuachana na vifaa vilivyopitwa na wakati.
Jiji la Tanga lina Kata 27, ambazo kwa pamoja zinazalisha zaidi ya Tani 217 za takataka kwa siku. Taka hizi huzalishwa katika kaya, biashara, viwanda, mifugo, n.k.
Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira, Ndg. Kizito Nkwabi anasema, mbali na Jiji kuongeza uwezo wake, lakini pia inashirikisha sekta binafsi, na tayari jambo hilo linafanyika katika Kata za Nguvumali, Pongwe na Maweni.
"Tayari tunawatambua wadhibiti taka 430, ambao hawa ni wadhibiti taka kwa mfumo wa urejerezaji taka kuwa mali, kuzirudisha taka kwenye mnyororo wa thamani ili zitumike tena kwa manufaa. Hakuna taka ambayo haiwezi kutumika tena." Amesema Ndg. Kizito.
Ili kupata mgawanyo mzuri wa gari za kubeba taka, Halmashauri imekuwa ikitoa ratiba ya magari ya kubeba taka kwa kila kata. Katika hili, Ndugu Kizito anatoa maombi kwa jamii;
"Niwaombe Viongozi na jamii kwa ujumla, kuhakikisha takataka zinawekwa katika vifaa maalum vya kuhifadhia taka, na watoe taka kwa mujibu wa ratiba ya siku ya kupita gari. Wafuate ratiba ya kupita gari. Lakini pia wasimpe taka mtu asiye rasmi, ambaye hajaidhinishwa na Halmashauri kufanya kazi hiyo. Mfano unampa taka mtu halafu anaziacha mtaa wa pili, hii sio sawa."
Lakini mwisho, Kizito anakumbushia wajibu wa wakazi kulipa huduma hiyo. Hii ni sawa na ule usemi wa 'haki huenda na wajibu'. Tulipe ada ya huduma hii ambayo kwa kaya ni Tsh. 2000 kwa mwezi, huku maeneo ya biashara yakiwa na viwango vyao kwa mujibu wa ukubwa na aina ya biashara.
Kwa pamoja tuweke Jiji letu kuwa safi.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.